
Haaland kukaa nje ya uwanja wiki saba
Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland atakuwa nje hadi wiki saba kutokana na jeraha la kifundo cha mguu alilopata katika ushindi wa robo fainali ya Kombe la FA Jumapili dhidi ya Bournemouth.
Raia huyo wa Norway alitolewa dakika ya 61 baada ya kufunga bao la kusawazisha huku City wakiendelea kuwafunga Cherries 2-1 na kutinga nusu fainali.
Video ilitumwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 akiondoka kwenye Uwanja wa Vitality kwa magongo na kifundo cha mguu wake wa kushoto kwenye kiatu cha kujikinga.
"Waliniambia madaktari wanasema kati ya wiki tano hadi saba," alisema Guardiola. "Kwa hivyo tunatumai mwisho wa msimu na kwa Kombe la Dunia la Klabu atakuwa tayari.
City ilisema Jumatatu kwamba Haaland angeonana na mtaalamu kuhusu jeraha hilo na wanatarajia "atakuwa sawa kucheza sehemu iliyosalia ya msimu huu ikijumuisha Kombe la Dunia la Klabu ya Fifa".
Haaland alikosa penalti na nafasi mbili kubwa siku ya Jumapili, lakini aligeuza krosi ya Nico O'Reilly kusawazisha mchezo kabla ya Omar Marmoush kufunga bao la ushindi.
Kombe la FA ndiyo nafasi pekee iliyosalia kwa City ya kutwaa taji msimu huu kufuatia kampeni ngumu ya Ligi Kuu ya England na kuondoka mapema kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Carabao.
Meneja Guardiola amelazimika kukabiliana na majeraha kwa wachezaji muhimu katika kipindi chote cha kampeni.
Kikosi chake kiko katika nafasi ya tano kwenye Ligi ya Premia, pointi moja nyuma ya Chelsea katika mbio za kuwania kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa.